Pinda: Deci batili

P.PindaWaziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema Kampuni ya Development Entrepreneurship For Community Initiative (DECI) ni ya upatu na inaendeshwa kinyume cha sheria za nchi. Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jana Dar es Salaam, Pinda alisema kutokana na hali hiyo, timu ya wataalamu kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Jeshi la

Polisi na Mamlaka ya Soko la Mitaji (DSE) inachunguza ili kujiridhisha na hatua zichukuliwe. Waziri Mkuu alisema hata hivyo tahadhari iliyotolewa na wataalamu hao kupitia vyombo vya habari kwa ajili ya wateja ni muhimu na kutaka kila mhusika azingatie kwani michezo ya upatu mwisho wake huwa ni mbaya.

Alisema Deci ilijiandikisha kwa Msajili wa Kampuni nchini (BRELA) Julai 25 mwaka jana, kama asasi ya kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo, lakini kinyume chake ikaanza kuchukua fedha kutoka kwa mteja mmoja na kumlipa mwingine kwa njia ya mzunguko.

Pinda alisema kwa kasi ya ajabu mpaka sasa Deci imekua na kufikia mikoa 18 nchini na jumla ya matawi 46 ikiwa na wateja 430,276 wenye jumla ya amana ya Sh bilioni 13.75. Hata hivyo alisema kwa mujibu wa uchunguzi, imebainika kuwa kampuni hiyo hadi Aprili 6 mwaka huu ilikuwa na amana ya Sh bilioni 1.83 tu katika akaunti zake kwenye benki kadhaa nchini.

Alisema hilo ndilo tatizo kubwa kwani hata kama ikitokea kampuni hiyo ikafa haitaweza kuwalipa wateja wake ambao wamepanda kwa mujibu wa utaratibu wake. "Hili kwa kweli kwa mchezo huu wa upatu ndilo linalotutia shaka, kwani amana ya wateja ni kubwa lakini fedha zao haziko benki na ikilinganishwa na zilizoko benki ni kidogo sana.

"Hii kama itatokea kampuni ikafa, kama ilivyo kawaida kwa upatu duniani kote, watashindwa kuwalipa wateja fedha zao," alisema Waziri Mkuu akitolea mifano ya Kenya, Marekani na Albania, ambako matatizo yalitokea kutokana na kufa kwa kampuni kama hizi. Kimsingi, Waziri Mkuu alisema kwa harakaharaka, upatu huu unaonekana kuwa na manufaa makubwa kwa watu kwani kwa utaratibu wa kupanda na kuvuna, kila apandaye mwanzoni anavuna fedha nyingi lakini baadaye jinsi unavyopanuka inakuwa shida kulipana.

Alisema tatizo ni kuwa fedha nyingi ziko nje ya mfumo wa benki na hivyo kuwa hatari zaidi likitokea tatizo lolote likiwamo hilo la kampuni kufa. "Deci ikifa leo na mali zake zote kukusanywa, bado haitakuwa na uwezo wa kuwalipa wanachama na hilo litasababisha vurugu kubwa nchini na serikali kulalamikiwa kuwa haikuifanya lolote, ingawa sasa wanaovuna hawalioni hilo," alisema Waziri Mkuu.

Akifafanua, alisema Deci haina uendelevu na hivyo kuwa tatizo kwa sababu inategemea zaidi idadi ya wanachama wapya ili kuwalipa wa zamani na hivyo ikifa wanachama wapya hawatapata kitu na hivyo kusababisha hasara na matokeo yake ni ghasia. Kuhusu sababu za kusajiliwa miaka mitatu iliyopita bila kuchukuliwa hatua na serikali, Pinda alisema BoT iliikubalia Deci kufanya shughuli zake kutokana na msingi wa usajili kuwa ilikuwa sawa na SACCOS na kwa imani hiyo hakukuwa na sababu za kuifuatilia sana.

Lakini baadaye, ilikiuka uendeshaji wake mpaka msamaria alipoishitua BoT mwaka huohuo kuwa wanafanya upatu badala ya makusudio yake, hivyo mawasiliano yakaanza mwaka jana. "Walianza kuwasiliana mwaka jana karibu wote wakitafuta maelezo, lakini Deci wakaanza kupiga chenga na mwaka jana mwishoni Mamlaka ya Mitaji nao wakashituka na kufuatilia...mwaka jana wote ulikuwa wa mawasiliano tu na ndipo sasa wakaona inazidi ndipo hatua zikaanza kuchukuliwa," alisema.

Hata hivyo, alisema bado yanaweza kufanyika mazungumzo na uongozi wa Deci kuona kama watakuwa tayari kurejea madhumuni waliyosajiliwa nayo ya kukopesha wajasiriamali, ingawa suala la uvunjaji wa sheria bado litakuwa mikononi mwa Polisi. Ila aliwataka wananchi kuelewa kuwa Deci haina chochote kinachohusiana na maono au ufunuo bali ni upatu kama mwingine.

Waziri Mkuu aliwataja wanahisa wa Deci kuwa ni Mchungaji Jackson Mtaresi mwenye hisa 12,800 (32%), Timotheo ole Loitinya hisa 6,400 (16%), Dominic Kigendi hisa 6,400 (16%), Samwel Mtaresi hisa 6,400(16) na Deci Africa Limited hisa 6,400 (16%) Kuhusu hali ya chakula na uchumi kwa ujumla nchini, Waziri Mkuu alisema hali si nzuri sana kama ilivyotarajiwa kutokana na baadhi ya maeneo kukosa mvua za vuli.

Hata hivyo, alisema ameiagiza BoT kuandaa taarifa na kuiwasilisha katika Kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge, ili iweze kujadiliwa na wananchi waelezwe hali halisi inavyokwenda na jinsi ya kukabiliana nayo.

Source:HabariLeo


back to top

Links

Advertising