Rais Kikwete aipongeza Stars

MtanzaniaRAIS Jakaya Kikwete amesema Taifa Stars imewatoa mchanga wa macho Watanzania na hasa mashabiki wa soka, kufuatia ushindi wa mabao 2-1 walioupata juzi mjini Khartoum, Sudan.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Mapinduzi(UVCCM), uchaguzi uliofanyika ndani ya ukumbi wa Kilimani mjini hapa.

Akizungumza na zaidi ya vijana 700 waliohudhuria mkutano huo kutoka mikoa yote nchini, Rais Kikwete alisema kitendo kilichofanywa na Stars ni cha kishujaa ambacho kinapaswa kuungwa mkono na Watanzania wote kwa ajili ya kuleta mshikamano katika medani ya michezo.

“Mtu anapofanya vizuri ni lazima umpongeze, ni jambo jema tu hili katika kumfanya mtu huyo ajione anapendeka, kwa hiyo ushindi wa Taifa Stars ni zawadi kwetu sote, hivyo ni lazima tuwapongeze kwa hicho walichokifanya tena ukizingatia walikuwa ugenini,’’ alisema Rais Kikwete huku akionekana mwenye tabasamu usoni.

Alisema ushindi huo ni heshima kubwa kwa nchi ya Tanzania ambayo kwa miaka mingi imekuwa msindikizaji wa nchi nyingine katika mashindano mbalimbali yaliyofanyika ndani na nje ya nchi, hali iliyopelekea kubatizwa jina la ‘kichwa cha mwendawazimu’.

“ Jamani, zamani timu yetu ilikuwa ikinyanyaswa sana na timu nyingine za Afrika hadi kufikia hatua ya kubatizwa jina la 'kichwa cha mwendawazimu' ambacho kila mtu anajifunzia kunyoa,l akini leo hii sisi tumekuwa ndiyo vinyozi wazuri na hivyo kutimiza ule usemi wa ‘wa kwanza atakuwa wa mwisho na wa mwisho atakuwa wa kwanza’,’’ aliongeza.

Alisema kuwa kiwango kilichoonyeshwa na Stars hivi karibuni ni dhahiri kwamba sasa nchi inaelekea mahali pazuri katika michezo na hasa mpira wa miguu, hivyo aliwataka wadau kuendelea kujitolea katika kuisaidia timu hiyo.

Aidha, Rais Kikwete aliahidi kuwa serikali itaendelea kumlipa kocha mkuu wa timu hiyo na kuihudumia timu ili kuendelea kuwatia moyo wachezaji pamoja na kocha na kuhakikisha kwamba inafanya vizuri katika fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani, Ivory Cost.

“Kwa matokeo haya ambayo yanatia moyo, sisi kwa upande wetu kama serikali tutaendelea kumlipa kocha, hatua ambayo tunaamini kwamba itasaidia katika kuleta ushindi zaidi ambao utakuwa ni furaha kwa Watanzania wote,” alisema Rais Kikwete.

Alisema kuwa wakati kocha Maximo akiwaita wachezaji wasio na majina kujiunga na kikosi chake na kuwaacha wale wenye majina, baadhi ya wananchi walionekana kulalamika na hasa wakati ilipotokea timu kufungwa na wapinzani wake, lakini yeye aliziba masikio kwa kuwa alikuwa anajua ni nini anachokifanya.

“ Nataka niwaambie kwamba wakati nazungumza na Balozi wa Brazil kwa ajili ya kumpata kocha, alinishauri kwamba hakuna haja ya kumchukua kocha kama Alberto Pereira kwa maelezo kuwa nchi ambayo bado ni changa kama ya kwetu mtu anayefaa kuifundisha timu ni Maximo, na nadhani sasa matokeo mnayaona,” alisema Kikwete huku akishangiliwa na ukumbi mzima.

Aidha aliwataka wadau wengine kujitokeza kwa wingi katika kuhakikisha kwamba wanaidhamini timu hiyo, ili kumfanya kocha na wachezaji kuwa na moyo wa kujituma zaidi wakati wa mazoezi pamoja na mashindano mbalimbali.

Source:HabariLeo

Links

Advertising