Pamba yaendelea kumezwa na mtikisiko wa uchumi Duniani
Baada ya dunia kuingia kwenye sereka za kukumbwa na athari za mtikisiko wa kiuchumi, mambo mengi yameendelea kuzungumzwa kuhusiana na athari zinazoendelea kujitokeza.
Watalaam wa mambo ya uchumi wanasema kuwa athari za mtikisiko huo huenda zikawa kuwa kubwa ingawa kuna juhudi za mazungumzo zinazoendelea miongoni mwa mataifa makubwa duniani kutafuta suluhisho la utatuzi wa hali hiyo.
Mataifa hayo yako kwenye mijadala ya kutafuta ni namna gani wanaweza kuokoa viwanda na taasisi zao za fedha ili zisiendelee kuathiriwa na mtikisiko huo, ingawa kazi ya mijadala hiyo imekuwa na kigugumizi cha hapa na pale.
Wakubwa hawa wanajihoji kutoka mioyoni mwao kuwa ni kipi wakifanye ili waweze kuendesha biashara zao na taasisi zao za fedha na wakati huo huo kuhakikisha kuwa wanakilinda kwa gharama yoyote chombo chao cha fedha (Benki ya Dunia) na taasisi zake dhidi ya mtikisiko huo.
Wako kwenye mijadala mizito ambayo inategemewa kuja na majibu juu ya nini hasa kifanyike.Biashara za mabenki zinajiendesha kwa kusuasua kutokana na kutokuwepo kwa mzunguko wa biashara ya fedha.
Tanzania nayo kama ilivyo nchi nyingine duniani nayo kwa kiwango fulani imetikisswa na hali hiyo,ingawa Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa haijaathiriwa kwa kiwango kikubwa na mtikisiko huo. Wananchi kwa upande mwingine kwenye maseneo mbalimbali nchini wameendelea kuhoji nini kitafuata mara baada ya hapo.
Ni kwa mantiki hiyo basi baadhi ya wasindikaji na wanunuzi wa zao la pamba kwa mikoa ya Kanda ya ziwa, wameshindwa kurejesha mikopo ya zaidi ya Shilingi bilioni 100 waliyokopa kutoka katika taasisi za fedha kwa lengo la kununulia pamba kwenye msimu wa kilimo wa mwaka 2008/09.
Wanunuzi na wasindikaji hao wanasema wameshindwa kurejesha mikopo hiyo pamoja na riba kutokana na kile walichokieleza kuwa ni kushuka kwa bei ya pamba katika soko la dunia kutoka St.82 hadi st.42 kwa ratili moja ya pamba na hivyo kujikuta wakiiuza pamba waliyoinunua kutoka kwa mkulima kwa sh.500 na kuiuza kwenye soko hilo. Wadau hao waliyasema hayo hivi karibuni jijini Mwanza kwenye kikao cha kutathimini maendeleo ya zao la pamba kwa mikoa ya Kanda ya ziwa inayolima zao hilo .
“Tunaiomba Serikali ichukue hatua za makusudi ili ione namna ya kutusaidia kulipa madeni haya tunayodaiwa na taasisi za fedha,ili tuendelee kuthaminiwa na taasisi hizo,na hivyo tuweze kuendelea kununua zao la pamba kwenye msimu ujao,” anaeleza mmoja wa wadau hao.
Mkutano huo uliohudhuriwa pia na Waziri wa Kilimo,Chakula na Ushirika Stephen Wassira,na kuhudhuriwa na wakuu wa mikoa na wilaya,wakuruigenzi watendaji,wawakilishi wa wakulima na watalaam wa kilimo ulipata fursa ya kujadili kwa kina matatizo yanayoikumba sekta ya zao la pamba.
Mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Mstaafu Issa Machibya mbali na kukiri kuwepo kwa udodoraji wa uchumi, alitoa wito kwa serikali kuangalia uwezekano wa kuwadhibiti wanunuzi machinga wa zao la pamba ambao kimsingi wanafanya biashara zao kwa kumyonya mkulima na bila ya kujali.
“Machinga hawa wamekuwa ni kero kubwa,hawajali utakuta wananunua pamba na wakati wa kuisafirisha pamba nyingi humwagwa barabarani,niiombe serikali iwatazame hawa kwani wanawakatisha tamaa wakulima wetu,” anasema Machibya.
Christopher Mwita Gachuma ambaye ni mdau na mnunuzi wa zao la pamba anatoa wito kwa serikali kuendelea kuiboresha mifumo yake mbalimbali ya ununuzi wa zao la pamba ukiwemo ule wa stakabadhi ghalani ili kuwanufaisha wote wanunuzi na wakulima.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Yohana Balele anakiri kuwa mifumo ya ununuzi wa zao la pamba karibu yote inafanana,anaishauri serikali kuangalia uwezekano wa kuja na mikakati itakayowawezesha wakulima kuendelea kupiga hatua zaidi.
Anakerwa na baadhi ya watendaji wanaosimamia vyama vya msingi na vya ushirika waone kuwa wanasimamia vyama vyao na hivyo kuviacha vinajiendesha kiholela ni kuwasaliti wakulima.
Akitolea mfano chama cha Ushirika cha Shinyanga (SHIRECU) anasema kuwa chama hicho kwa jinsi ambavyo kinapokewa na jamii ya wakulima kina hali ambayo hairidhishi na anatoa ushauri juu ya utendaji kazi wa SHIRECU.
“Imefika mahali nasema kwanini jina la SHIRECU lisibadilishwe ili litoke masikioni kwa wakulima,ili tuone kama tutapata kitu kipya cha kuendesha ushirika,”anasema Balele.
Mbunge wa Jimbo la Meatu (CCM) Mkoani Shinyanga Salum Khamis Salum yeye anaitaka serikali iwalipe fidia wakulima wa zao la pamba kutokana na kuathiriwa na mtikisiko wa dunia.
Salum anasema kuwa soko na bei ya pamba limeonekana kuyumba kutokana na kuwepo kwa mtikisiko wa dunia na kuitaka serikali kuingilia kati (to intervine) ili iweze kuwalipa fidia wakulima kama ambavyo zinafanya badhi ya nchi nyingine akiitolea mfano nchi ya Uganda .
“Asilimia kubwa ya wakazi wa Kanda ya ziwa wanategemea kilimo cha zao la pamba, na serikali isiendelee kuukumbatia ushauri wa IMF na Benki ya Dunia na kuyumbishwa na taasisi hizi, hawa ndio waliosababisha kuwepo kwa mtikisiko wa uchumi duniani na ndio wanaopaswa kubebeshwa mzigo huu na sio wakulima,” anaeleza Salum na kusisitiza kuwa madai kuwa kuporomoka kwa soko la zao la pamba kunatokana na mtikisiko huo sio ya kweli.
“Mbona Uganda wakulima wao wa pamba hawaathiriki na hali hii ya mtikisiko wa uchumi wa dunia, wabunge wote wa kanda ya ziwa tumeazimia kupambana na swala hili ili kuhakikisha kuwa serikali inawalipa fidia wakulima dhidi ya mtikisiko huu,” anaeleza Salum.
Anaishauri serikali kuondokana na tofauti za kiitikadi ili kuhakikisha swala hilo linapewa umuhimu wa kipekee kwa kuwajibika kwa wakulima kwa manufaa ya ya maendeleo ya wakulima na taifa kwa ujumla.
Waziri wa Kilimo,Chakula na Ushirika Stephen Wasira anakiri kuwepo kwa mtisiko huo,lakini anawahakikishia wakulima kuwa serikali itanunua pamba yote itakayokuwa ikizalishwa na wakulima hivyo wasiwe na hofu yoyote ile.
Source:HabariLeo
Links 