Bakwata yatengua hukumu ya katibu wa mkoa

BAKWATABARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), makao makuu limetamka rasmi kuwa kikao kilichokaa na kufanya maamuzi ya kumfukuza Katibu wa Mkoa wa Arusha na viongozi sio halali kwa mujibu wa katiba ya Bakwata kifungu 52/11.

Kutokana na hali iliyojitokeza mkoani Arusha, Mufti wa Tanzania, Sheikh Issa bin Shaaban Simba, amesema viongozi wote waliotajwa kuwa wamefukuzwa na kikao hicho batili bado, wanatambulika ni viongozi halali na Baraza halitambui maamuzi yaliyofanywa na kikao hicho.

Kauli hiyo imekuja baada ya gazeti moja la kila siku kuripoti kuwa, Bakwata Mkoa wa Arusha limemvua wadhifa wake katibu wa mkoa, Ally Mzee na viongozi wengine wa ngazi ya mtaa kwa tuhuma za ufujaji wa fedha.

Viongozi waliotajwa kuwa wamefukuzwa ni Sheikh Abdulrahman Salim, Mohamed Nyagawa, Mbaraka Mtonyi, Sheikh Rajab Kiungiza na mwalimu Yunusi.

Barua ya kuwafukuza viongozi hao ilisainiwa na Mwenyekiti wa Baraza la Masheikh mkoani Arusha, Sheikh Adam Chola na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bakwata, Mkoa wa Arusha, Alhaj Iddy Kateta.

Mufti Simba alisema kwamba, Baraza linafuatilia kwa karibu hali ya uongozi katika Mkoa waArusha na Waislamu wa Arusha wanaombwa kuwa watulivu na kutumia fursa ya uchaguzi ambao sasa unaendelea ili kuweka madarakani viongozi bora wanaohitajika katika ngazi mbalimbali kuanzia ngazi ya msikiti.

Wakati huo huo, Nora Damian anaripoti kutoka jijini Dar es Salaam kwamba, maandamano ya Waislamu yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Ijumaa wiki hii kupinga kiwanja chao cha Chang’ombe kuuzwa kinyemela yamesitishwa.

Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili jana, Katibu wa Baraza la Habari la Kiislamu Tanzania (Bahakita), Sheikh Said Mwaipopo alisema, wamesitisha maandamano hayo baada ya Mufti Mkuu Sheikh Issa Simba kutoa tamko kuhusu kiwanja hicho.

Source:HabariLeo


back to top

Links

Advertising